Home KITAIFA Tunataka kazi za serikali zifanyike makao makuu ya nchi-Dk.Mwigulu

Tunataka kazi za serikali zifanyike makao makuu ya nchi-Dk.Mwigulu

Asisitiza Taasisi za Serikali zinapaswa kufahamu kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inataka kazi zote zifanyike makao makuu ya nchi ili kusogeza huduma karibu na Wananchi.

Amesema hayo leo Januari 22, 2026 alipotembelea Ofisi za Wizara ya Maji na Wizara ya Madini zilizopo mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

“Ninawapongeza sana, mmehamia Makao Makuu, taasisi zote za Serikali zinapaswa kutambua kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma, na huduma zote zinapaswa kutolewa hapa, hii sio kambi na wala hatutakuwa na Makao Makuu mbili zilizo sambamba”.

Pia, Dk. Mwigulu ameziagiza Taasisi zote ambazo zimeshakamilisha ujenzi wa majengo katika makao makuu kuyatoa majengo hayo kwa Taasisi ambazo haziwajibiki kuhamia Dodoma lakini bado zimepanga.

“Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu mwelekeze Katibu Mkuu atengeneze timu ifanye tathmini ya majengo yote ya Serikali yaliyoko Dar es Salaam ambayo hayana matumizi ili tuyagawe kwa taasisi nyingine ambazo zimepanga, angalia Serikali ina majengo yasiyotumika,”amesema.

Amesema kwa kuwa Ofisi za Serikali zipo karibu, hivyo hakuna haja ya kuandikiana barua za masuala mbalimbali ya utekelezaji badala yake waweke mpango wa kutembeleana katika ofisi husika ili kutatua jambo lilikokwama kwa wakati”

Akizungumza na Watumishi wa Wizara ya Maji, Dk. Mwigulu amewataka kwenda katika hatua ya kukomesha kabisa upotevu wa maji.

“Tunapokwenda kutekeleza dira mpya tunatakiwa twende na ustaarabu na miundombinu inayomuhakikishia mtanzania uhakika wa kupata maji”

Akizungumza wakati akikagua majengo ya Wizara ya Madini,Dk. Mwigulu amewataka wataalam wa madini kuendeleza jitihada kwenye tafiti za madini ili kujua utajiri uliopo nchini.

Kwa Upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi ya kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi kubwa zilizowahakikishia watumishi mazingira mazuri ya ufanyaji kazi.

Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo umesaidia kutekeleza maagizo ya Rais Dk. Samia ya kuhakikisha huduma zote zinatolewa katika eneo hilo, watanzania wote waliokuwa wanapata changamoto ya kupata huduma kwasasa changamoto hiyo imeondoka”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here