Na Mwandishi Wetu, Tanga
SHULE ya Msingi Mwakidila, iliyopo Kata ya Tanga, Halmashauri ya Jiji la Tanga, imefanyiwa maboresho makubwa ya miundombinu na ufundishaji kupitia Mradi wa BOOST, hatua iliyoongeza ufanisi wa elimu ya awali na msingi pamoja na kuvutia ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Januari 28, 2026 Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Hadija Bakari, amesema Mradi wa BOOST umeleta mageuzi makubwa katika mazingira ya kujifunzia na kufundishia, sambamba na kuboresha ubora wa elimu shuleni hapo.
Amesema shule ilipokea jumla ya Shilingi Milioni 112.3, fedha zilizotumika kujenga madarasa mawili ya elimu ya awali, matundu manne ya vyoo, kukarabati vyumba sita vya madarasa na matundu 14 ya vyoo pamoja na kujenga vyumba vitatu vipya vya madarasa.
“Kupitia Mradi wa BOOST, shule imenufaika pia na vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta 12 za mezani, kompyuta mpakato moja na kinakilishi kimoja, ambavyo vimeongeza ubora wa ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi,” amesema Hadija.
Ameongeza kuwa vifaa hivyo vimewawezesha walimu kupakua na kutumia nyenzo mbalimbali za kufundishia pamoja na kurahisisha ujazaji wa taarifa katika mifumo ya Serikali ikiwemo Mfumo wa Taarifa za Wanafunzi (SIS) na Mfumo wa Huduma za Watumishi (ESS).
Kwa upande wake, Mwalimu wa Elimu ya Awali katika shule hiyo, Saumu Mahamud Alli, amesema maboresho hayo yameleta mabadiliko chanya makubwa kwa watoto wa elimu ya awali.

“Kabla ya utekelezaji wa mradi huu, shule ilikuwa na uhaba mkubwa wa madarasa hali iliyosababisha msongamano wa wanafunzi. Kupitia madarasa mapya, watoto sasa wanajifunza katika mazingira salama, tulivu na rafiki, jambo linaloongeza ufanisi na uelewa wao,” amesema Saumu.
Ameeleza kuwa uwepo wa vifaa vya TEHAMA umeongeza uwezo wa wanafunzi kujifunza masomo ya TEHAMA na Sayansi kwa vitendo, hali inayochochea hamasa ya kujifunza na kuongeza ushiriki wao darasani.
Aidha, amesema maboresho ya miundombinu yamechangia kupungua kwa utoro wa wanafunzi, tofauti na awali ambapo majengo chakavu yalikuwa kikwazo kikubwa cha mahudhurio.
Naye Hadija amesema maboresho yaliyofanywa kupitia Mradi wa BOOST yamesababisha ongezeko la idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika shule hiyo kutokana na kuvutiwa na ubora wa majengo na mazingira ya shule kwa ujumla.
Kwa pamoja, walimu wa Shule ya Msingi Mwakidila wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwekeza katika elimu ya awali na msingi, wakisema uwekezaji huo ni msingi imara wa maendeleo ya elimu na taifa kwa ujumla.



