Home KITAIFA BoT: Hatuuzi dhahabu kufadhili miradi ya serikali

BoT: Hatuuzi dhahabu kufadhili miradi ya serikali

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mtandaoni ya kijamii zikidai kuwa BoT ina mpango wa kuuza sehemu ya hifadhi yake ya dhahabu ili kufadhili miradi ya kimkakati ya serikali.

Pia BoT imesema haina mpango wa kuuza sehemu ya hifadhi yake ya dhahabu kwa ajili ya kufadhili miradi ya kimkakati ya serikali, bali inakusudia kuuza iliyozidi kiwango kilichoidhinishwa ili kurejesha uwiano sahihi wa hifadhi ya dhahabu hiyo katika nchi.

Akizungumza leo Januari, 30 2025 jiji Dar es Salaam na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro, amesema hatua inayotekelezwa kwa sasa ni mpango wa kuuza dhahabu iliyozidi kiwango hicho kwa mujibu wa maamuzi ya bodi.

“Bodi ya BoT imeidhinisha hifadhi ya dhahabu isiyozidi thamani ya Dola za Marekani bilioni mbili, hata hivyo hadi sasa hifadhi hiyo imefikia takribani dola bilioni 3.2, hali inayolazimu kupanga kuuza ziada iliyopo ili kubaki ndani ya kiwango kilichoidhinishwa,” ameeleza.

Amefafanua kuwa fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo hayo zitaelekezwa katika uwekezaji kwenye masoko ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato ya uwekezaji wa BoT, na si kufadhili miradi ya serikali. Ameongeza kuwa matumizi yoyote ya uwekezaji wa BoT kwa ajili ya serikali yanahitaji idhini ya Bunge.

Akaro amesema kuwa uamuzi wa kuuza dhahabu unatokana na haja ya kudhibiti vihatarishi vya kifedha,akieleza kuwa BoT inapouza dhahabu hununua Dola za Marekani ili kuhakikisha benki haijiweki kwenye hatari zisizoweza kudhibitiwa.

Ameeleza zaidi kuwa hadi Januari 29, 2025, BoT ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni zenye thamani ya dola bilioni 6.5, ambapo kati ya hizo dhahabu ilikuwa na thamani ya dola bilioni 1.2, Dola za Marekani bilioni 3.5, na sarafu ya China (Yuan) zenye thamani ya dola milioni 735.

Kwa mujibu wa Akaro, BoT hununua dhahabu kila siku, na katika kipindi cha miezi mitano iliyopita imenunua wastani wa karibu tani mbili za dhahabu kila mwezi, sawa na asilimia 20 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini na kuuzwa nje.

Amesisitiza kuwa ziada ya hifadhi ya fedha za kigeni hutumika pia katika kugharamia mahitaji ya serikali ya manunuzi ya nje, akifafanua kuwa serikali hununua fedha za kigeni kutoka BoT kwa kutoa shilingi badala ya kwenda katika benki za biashara.

Aidha, amesema BoT ina majukumu ya kuingiza fedha za kigeni kwenye soko la ndani ili kusaidia upatikanaji wa fedha hizo kwa wananchi, ambapo kwa mwaka 2025 benki hiyo iliingiza sokoni takribani dola milioni 401, hatua iliyosaidia kuimarika kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here