Home AFYA Bima ya Afya kwa Wote kuyafikia makundi maalum ya kijamii-Mchengerwa

Bima ya Afya kwa Wote kuyafikia makundi maalum ya kijamii-Mchengerwa

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote umeendelea kuwafikia makundi maalum ya kijamii, yakiwemo wafugaji, wakulima, wasanii, waendesha bodaboda pamoja na wachimbaji wadogo.

Ameyasema hayo Februari 2, 2026 jijini Dar es Salaam Mchengerwa wakati akizungumza katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Ukumbi wa Karimjee.

Amesema dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa sahihi na kwa wakati kwa kutumia lugha rahisi na njia zinazowafikia wananchi moja kwa moja, ili kuongeza uelewa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote na kuhamasisha usajili wa wananchi wengi zaidi.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema mpango huo umezingatia makundi yenye uhitaji maalum, yakiwemo wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu, ambapo makundi hayo yataendelea kupatiwa huduma za matibabu bila malipo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali.

“Serikali inaendelea kuhakikisha taarifa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote zinamfikia kila mwananchi kwa kuingiza ajenda ya bima katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi. Hatua hiyo inajumuisha matumizi ya sanaa, wasanii pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano katika kampeni za uhamasishaji ili kuongeza mwitikio wa wananchi kujiunga na mpango huu,”amesema.

Vilevile Mchengerwa, amewatoa hofu Watanzania kuhusu usalama na ubora wa dawa za kufubaza makali ya UKIMWI (ARVs) zitakazozalishwa mkoani Arusha, akifafanua kuwa serikali imechukua umiliki wa kiwanda hicho kwa zaidi ya asilimia 70.

Amekanusha uvumi uliosambaa mitandaoni kuwa kiwanda hicho kimekabidhiwa kwa wazalishaji waliowahi kuhusishwa na dawa feki huko nyuma.

Amebainisha kuwa kupitia Msajili wa Hazina, serikali sasa ndiyo mmiliki mkuu na msimamizi wa kiwanda hicho, tofauti na awali kilipokuwa chini ya umiliki wa watu binafsi kwa asilimia kubwa. Amesema serikali imejipanga kuhakikisha kiwanda hicho kinakidhi viwango vya kimataifa vya uzalishaji bora wa dawa.

“Kwa hiyo niwatoe hofu Watanzania kwa mipango na maandalizi tuliyojipanga nayo hakutakuwa na dawa feki itakayozalishwa katika kiwanda hiki ambacho sasa ni kiwanda kinachomilikiwa na serikali kwa zaidi ya 70%. Kwa hiyo waandishi wa namna hii ambao pengine wanajizolea umaarufu kwa kuandika habari feki ni vyema kabla hawajaandika warudi ndani ya serikali na sisi ndani ya serikali milango yetu iko wazi”, amesema Waziri Mchengerwa.

Ameeleza kuwa serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Viwanda vya Dawa (PIAT), ambacho tayari kimezungumza na zaidi ya kampuni 40 kutoka mataifa 28 duniani, ikiwemo Ujerumani, Uingereza, China, na India. Lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa bora barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here