Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta zitakazotumika nchini kuanzia Februari 4, 2026.

Taarifa hiyo inaonesha kushuka kwa bei ya dizeli kwa kiwango kikubwa kwa mafuta yaliyopokelewa katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 4 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Mwainyekule, bei ya rejareja ya dizeli imepungua kwa Sh 90 kwa mafuta yaliyopokelewa Dar es Salaam.
Katika bandari ya Tanga, dizeli imeshuka kwa Sh 25, huku Mtwara ikishuhudia punguzo la Sh 24 ikilinganishwa na bei za mwezi Januari 2026.

Aidha, bei ya mafuta ya taa nayo imepungua kwa Sh 17 Dar es Salaam, Sh 14 Tanga na Sh 93 kwa bandari ya Mtwara.
Kutokana na mabadiliko hayo, bei ya petroli kwa mwezi Februari 2026 ni Sh 2,788 kwa Dar es Salaam, Sh 2,849 kwa Tanga na Sh 2,881 kwa Mtwara.
Kwa upande wa dizeli, bei ni Sh 2,701 Dar es Salaam, Sh 2,762 Tanga na Sh 2,807 Mtwara.
Mafuta ya taa yanauzwa kwa Sh 2,881 Dar es Salaam, Sh 2,794 Tanga na Sh 2,838 kwa Mtwara.
EWURA imeeleza kuwa, kwa mwezi Februari 2026, gharama za kuagiza mafuta katika bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 1.88 kwa petroli na asilimia 1.65 kwa mafuta ya taa.
Hata hivyo, gharama za kuagiza dizeli katika bandari hiyo zimepungua kwa wastani wa asilimia 5.10.
Katika bandari ya Tanga, gharama za kuagiza petroli na dizeli zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.62.
Kwa upande wa bandari ya Mtwara, gharama za kuagiza petroli zimepungua kwa wastani wa asilimia 9.24.
EWURA pia imesema wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umeongezeka kwa asilimia 1.86.
Wakati huo huo, EWURA imewakumbusha wauzaji wa mafuta nchini kutoa stakabadhi za mauzo kwa wateja wao.
Stakabadhi hizo zinapaswa kuonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa pamoja na bei kwa lita.
Vilevile, vituo vyote vya mafuta vimetakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana wazi.
EWURA imesisitiza kuwa kushindwa kutekeleza agizo hilo ni kosa kisheria na wahusika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.



