Home BIASHARA Dk.Mwigulu ataka mikakati ya kulinda viwanda vya ndani

Dk.Mwigulu ataka mikakati ya kulinda viwanda vya ndani

Mwandishi Wetu, Pwani

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amezitaka Taasisi za udhibiti za Serikali kuweka kipaumbele katika kulinda viwanda vya ndani na biashara badala ya kuwa kikwazo katika kufikia mafanikio.

Amesema kuwa haitakuwa rahisi kulinda viwanda na biashara za ndani kama Tanzania itakuwa jalala la bidhaa kutoka nje.

Amesema hayo leo Alhamisi Februari 12, 2026 alipozindua kiwanda cha mabati cha Lodhia kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.

“Wizara ya fedha hakikisheni hamtoi msamaha wala unafuu wa kodi katika bidhaa za nje ambazo zinapatikana ndani ya nchi. Toeni unafuu wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kama uzalishaji ndani ya nchi hatujitoshelezi,”amesema.

Aidha, Dk. Mwigulu ameitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania na Vyombo vya ulinzi kuhakikisha hakuna bidhaa za magendo zinazoingia nchini.

“Taasisi zote na vyombo vya ulinzi simamieni uingizaji wa bidhaa ndani na ufuate utaratibu, msipofanya hivyo mtaua uwekezaji unaofanywa ndani,”amesema.

Amesema kuwa Sekta binafsi ni mdau mkubwa katika maendeleo na injini ya kuchachusha utekelezaji wa miradi na ndio maana Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika viwanda na ufanyaji wa biashara.

“Wahitimu zaidi ya milioni mbili kila mwaka katika ngazi mbalimbali wanaingia katika soko la ajira, ni lazima tukuze sekta binafsi ambayo inauhakika wa kutoa ajira kwa wingi kwa watoto wa Kitanzania, maana yake ni lazima tulinde na tuvutie uwekezaji,”amesema.

Pia ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza kasi ya kuwezesha miundombinu ya kuongeza matumizi ya gesi katika uzalishaji Viwandani

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za makusudi za kulinda viwanda vya ndani na kuweka mazingira mazuri ya kuongezeka vingine.

Aidha, amesema kuwa uwepo wa kiwanda cha mabati cha Lodhia unalihakikishia Taifa soko la ndani la uhakika “Ninawapongeza sana kwa uwekezaji huu, sisi tunawahakikishia ushirikiano wa kutosha katika uwekezaji wenu nawapongeza pia kwa kuamua kuishi dhana ya uchumi wa viwanda.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here