Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ametoa onyo kali kwa Watanzania, hususan vijana, wanaojihusisha na biashara ya sarafu za kidijiti (cryptocurrencies) akibainisha kuwa biashara hiyo ina vihatarishi vingi kuliko faida kutokana na kukosa usimamizi rasmi.

Akizungumza katika mahojiano na Crown TV, Gavana Tutuba ameeleza kuwa chimbuko la sarafu hizo ni mbinu ya kukwepa (bypass) mifumo rasmi ya udhibiti wa kifedha inayoratibiwa na serikali na taasisi za kimataifa kupitia Benki Kuu.
Amefafanua kuwa tofauti ya msingi kati ya fedha rasmi (kama Shilingi ya Tanzania) na sarafu za kimtandao (Cryptos) hivyo Benki Kuu inapochapisha fedha, inafanya hivyo kulingana na shughuli halisi za kiuchumi zilizotekelezwa nchini, jambo linaloifanya Benki Kuu kuwa mdhamini wa mwisho wa thamani ya fedha hiyo.
“Tukichapisha tunaingiza Shilingi ya Tanzania kulingana na shughuli za kiuchumi zilizotekelezwa kwenye uchumi wa Tanzania. Lakini wakati huo huo siku mtu akihitaji ile shilingi yake anaweza akaja kuipata Benki Kuu. Sasa hatari iliyopo kwa hao wanaotengeneza hizo labda cryptos, wao wanakuwa hawana shughuli za kiuchumi zinazolingana na thamani ya zile coins au cryptos walizoingiza kwenye uchumi. Ndio maana ukitaka kuzipata sasa ukitaka kucash out, hauwezi ukazipata,” ameeleza Gavana Tutuba.
Moja ya hatari kubwa iliyoibuliwa na Gavana Tutuba ni ugumu wa kubadilisha sarafu hizo kuwa fedha taslimu pindi mtumiaji anapozihitaji. Kwa kuwa hazina mhimili wa kiuchumi unaoeleweka, thamani yake inaweza kupotea au mtumiaji akashindwa kuziuza ili kupata fedha halisi, tofauti na mifumo ya kibenki inayotambulika kisheria.
Licha ya kuwepo kwa aina mbalimbali kama Bitcoin na Stable coins, amesisitiza kuwa zote zina misingi inayofanana ya kutokuwa na udhibiti. BoT inaendelea kuwashauri wananchi kutojihusisha nazo hadi hapo utaratibu mwingine utakapoelekezwa, huku ikisisitiza kuwa jukumu la kulinda thamani ya fedha na njia ya kubadilisha fedha linabaki mikononi mwa taasisi rasmi za kisheria.
Ametoa wito kwa vijana kutokukimbilia fursa za kidijiti bila kufanya uchunguzi wa kina kwani wengi wanaingia kwenye mifumo hiyo bila kufahamu undani wake.



