Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Serikali imepiga hatua kubwa za maendeleo katika siku 100 za uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaonekana wazi katika sekta za uchukuzi, anga, reli, bandari na utalii.

Msigwa ametoa taarifa hiyo leo, Februari 26, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua na kueleza utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini, Lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Ameeleza kuwa mkutano huo umefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa makusudi, kuonesha uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya anga.
“Mchango wa sekta ya uchukuzi katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024”,amebainisha Msigwa.
Akizungumzia sekta ya viwanja vya ndege,amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inaendelea kutekeleza miradi ya zaidi ya shilingi trilioni 1.154 kwa lengo la kuboresha miundombinu, usalama na uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo. Mashine 13 za kisasa za ukaguzi zimefungwa katika viwanja mbalimbali ili kuruhusu huduma za saa 24.
Aidha ameongeza kuwa Miradi hiyo inahusisha upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Arusha, Moshi, Mwanza, Serengeti, Kyabajwa, Msalato, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Sumbawanga. Aidha, jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere limekamilika, hatua inayoongeza hadhi ya kidiplomasia ya nchi.
“Kutokana na maboresho hayo, mashirika saba mapya ya kimataifa yameanza safari nchini, yakiwemo Air France, South African Airways na Saudia. Hatua hiyo imeongeza ushindani, kurahisisha safari na kukuza utalii pamoja na biashara za kimataifa.”amesema Msigwa.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa mwaka wa fedha 2024/2025 kulikuwa na safari 149,835 za ndege, abiria milioni 5.25 na tani 37,683 za mizigo, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Katika nusu ya mwaka Julai–Desemba 2025 pekee, safari na idadi ya abiria zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 9 hadi 10, kuashiria ukuaji endelevu wa sekta hiyo.
Kwa upande wa Kampuni ya Ndege Tanzania, (ATCL) amesema Serikali imeendelea kuimarisha shirika hilo kwa kununua ndege mpya ikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner, na kufanya jumla ya ndege kufikia 16. Shirika limepanua safari zake kutoka vituo 23 mwaka 2020/21 hadi vituo 33 mwaka 2025/26, likiongeza idadi ya abiria hadi zaidi ya milioni 1.17 mwaka 2024/25.
Katika sekta ya reli, amesema Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye kilomita 1,219. Kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma tayari kinatoa huduma, huku zaidi ya abiria milioni 4.6 na tani 52,305 za mizigo zikiwa zimesafirishwa tangu kuanza kwa huduma.
Aidha, Serikali imesaini mkataba wa kufufua reli ya Tanzania–Zambia Railway Authority kwa kushirikiana na Zambia na kampuni ya CCECC ya China, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa biashara za kikanda na kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam.
Katika sekta ya bandari, amesema upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na miradi ya maziwa makuu inaendelea, huku mapato ya forodha yakiongezeka hadi trilioni 8.256 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025. Serikali pia imeimarisha usalama wa usafiri wa majini kwa kujenga Kituo cha MRCC Ziwa Victoria na kununua boti maalum za uokoaji.
Kwa upande wa utalii, Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa kupitia vivutio kama Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mlima Kilimanjaro, huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa asilimia 10.2 mwaka 2025. Tanzania pia imeshinda tuzo kadhaa za World Travel Awards, ikithibitisha nafasi yake kama kitovu cha utalii barani Afrika na duniani.



