Home KITAIFA WAZIRI MAVUNDE AKUTANA NA MWENYEKITI WA BODI YA EITI JIJINI DAR ES...

WAZIRI MAVUNDE AKUTANA NA MWENYEKITI WA BODI YA EITI JIJINI DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu@Lajiji Digital

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amekutana na kufanya kikao kifupi na Mwenyekiti wa Bodi ya EITI Rt. Helen Clark katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar Es Salam.

Pia, kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI CPA Ludovick Utouh na Katibu Mtendaji wa TEITI Bi Mariam Mgaya pamoja na viongozi kutoka Wizarani.

Akizungumza katika kikao hicho Mavunde amesema amefurahishwa na ujio huo na kueleza kuwa ni wa kihistoria ikiwa ni ushirikishwaji wa Sekta ya Madini katika shughuli za Uwazi na Uwajibikaji.

Aidha, kikao hicho kimekubaliana kuwa Wizara ya Madini ikishirikiana na Asasi za Kimataifa ya EITI itatimiza kikamilifu mahitaji ya matakwa ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji katika shughuli mbalimbali za Usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia nchini.

Pia, Mavunde amesisitiza kwamba maoni yaliyotolewa katika ripoti ya Tathmani ( Validation Report ) kuhusu Uwazi na Uwajibikaji katika nchi ya Tanzania iliyofanyika mwaka 2023 yatafanyiwa kazi kikamilifu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI CPA. Ludovick Utouh kwa niaba ya Katibu Mtendaji amesema dhana ya kuweka uwazi taarifa na takwimu mbalimbali za Sekta ya Uziduaji ni kuhakikisha kuwa Rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi na kuahidi kuwa TEITI itatoa ushirikiano katika kutekeleza Matakwa hayo.

Ujumbe huo wa EITI ukiongozwa na Rt. Helen Clark utapata wasaa wa kukutana na Dk. Samia Suluhu Hassan leo Aprili 04, 2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here