Home KITAIFA DK. BITEKO AKUTANA NA BALOZI MPYA WA UINGEREZA NCHINI.

DK. BITEKO AKUTANA NA BALOZI MPYA WA UINGEREZA NCHINI.

📌Tanzania na Uingereza Kuimarisha Ushirikiano katika Sekta ya Nishati

Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko Septemba 6, 2024 jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na balozi mpya wa Uingereza nchini, Marianne Young.

Lengo la mazungumzo hayo likiwa ni kujitambulisha kwa balozi huyo pamoja na kujadili masuala ya kipaumbele ya ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza katika sekta ya nishati.

Aidha katika mazungumzo hayo, Dk.Biteko amepongeza ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Uingereza katika sekta mbalimbali hususan sekta ya nishati kupitia ufadhili wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 11.16 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Songas kupitia taasisi zake za mitaji za Shirika la UK Export Finance (UKEF) na Shirika la Uwekezaji la Uingereza (BII).

‘‘Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika sekta ya nishati sambamba na kuikaribisha sekta binafsi kutoka nchini Uingereza kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati hususan nishati safi ya kupikia na nishati mbadala, ’’ amesema Dk. Biteko.

Kwa upande wake, Balozi Young, ameipongeza Tanzania kwa uongozi wake katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika na kusema kuwa nchi yake itaendelea kuunga mkono sekta ya nishati nchini.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Denis Londo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here