Dar es Salaam
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na ubongo Muhimbili (MOI) imehitimisha kambi maalum ya upasuaji wa kurekebisha kibiongo ambapo watoto 13 wamefanyiwa upasuaji huo kwa mafanikio makubwa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Laurent Lemeri Mchome amesema leo Februari 28, 2025 kuwa kukamilika kwa kambi hiyo kunafungua milango kwa watoto wenye ulemavu wa kibiongo kupata matibabu ya kibingwa na viungo vyao kurejea katika hali ya kawaida.
“Mafanikio ya kambi hii ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya Sita ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha taasisi ya MOI kuwa na vifaa tiba vya kisasa ambavyo vinarahisisha kufanya upasuaji wa kibingwa na kibobezi wa Mifupa, mgongo , ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na kusomesha wataalam,” amesema Dk. Lemeri.
Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa Watanzania wote kuwa huduma za upasuaji wa mgongo kibiongo zinaendelea katika taasisi hiyo, hivyo wazazi wameombwa kuendelea kuwapeleka watoto ili wapate matibabu hayo mapema.

Mratibu wa kambi hiyo Dk. Bryson Mcharo amesema kuwa watoto 13 wamefanyiwa upasuaji huo wa kurekebisha kibiongo katika kambi hiyo maalum kwa ushirikiano wa vyuo vikuu vya Ramallah cha nchini Palestine na Toledo- Ohio cha nchini Marekani.
“Mpaka sasa hivi tumefanyia upasuaji watoto 13 tangu Jumatatu (Februari 24, 2025), watoto waliokuwa na umri chini ya miaka 10 walikuwa wanne, kuna mmoja alifanyiwa upasuaji wa kitaalam zaidi, wanawakewa vyuma vya ndani lakini vinaruhusu kuongezeka urefu wako,” amesema Dk. Mcharo
Dk. Mcharo ametoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye kibiongo kuwawahisha hospitali ili kufanyiwa uchunguzi mapema kuepusha kufanyiwa upasuaji usiokuwa wa lazima.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa kambi hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Ramallah cha nchini Palestine na Chuo Kikuu cha Toledo- Ohio_ Marekani, Profesa Alaaeldin Azmi Ahmad amesema kuwa wataendelea kushirikiana na MOI ili kuwajengea uwezo wataalam hao na kuifanya taasisi hiyo kuwa Kituo cha umahiri cha mafunzo ya upasuaji wa kurekebisha kibiongo barani Afrika.