Tanga
MWENYEKITI wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Seleman Moshi Kakoso amezungumzia umuhimu wa ujenzi wa miundombinu mkoani Tanga kuwa jumuishi ili kuleta tija na maendeleo ya haraka.

Akizungumza leo Mach, 13, 2025 mara baada ya kamati yake kukagua upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Tanga, uboreshaji wa reli na Bandari Kakoso amesema mafanikio ya uwekezaji wa miradi hiyo yataleta tija ikiwa yatakuwa jumuishi.
” Tanroads, TRC na Bandari hakikisheni mipango yenu ya ujenzi inaungana mkono ili ufanisi wa bandari uendane na ujenzi wa barabara na reli na hivyo kuleta tija,” amesema Kakoso.

Amesisitiza upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Tanga kiendane na ukuaji wa fursa za uwekezaji wa mkoa huo ili utoe huduma bora na zakisasa.
“Hakikisheni ujenzi unakamilika kwa wakati na Serikali inapata thamani ya fedha kwa kazi itakayofanyika”, amesema Kakoso.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Wizara itazingatia ushauri wa kamati ili kuhakikisha mkoa wa Tanga unafunguka kimiundombinu na kuifungua pwani yote ya Afrika Mashariki.