Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua Kampeni Kabambe ya Msimu wa Sikukuu kwa ajili ya kuwazawadia wateja wake wanaofanya malipo kwa kutumia kadi ya Popote Visa, ambapo watapata rejesho la 10% kwa kila muamala unaokidhi vigezo vilivyowekwa na benki.

Akizungumza leo Disemba, 12 2025 jijini Dar es Salaam katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa TCB, Alex Dwashi amesema kampeni hii inaonyesha dhamira ya benki kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali, hasa katika msimu wa sikukuu ambapo matumizi ya kifedha huongezeka.
Naye, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Kibunifu wa TCB, Jesse Jackson, amesema rejesho la asilimia 10 kwa miamala ya Popote Visa limekusudiwa kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo isiyotegemea fedha taslimu, ambayo ni salama na rahisi zaidi kwa wateja.

Ameongeza kuwa benki inaendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha huduma na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati TCB, Lilian Mtali ameeleza kuwa hatua hii inatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja na maboresho ya kimkakati ndani ya benki, huku ikichangia kusukuma mbele ajenda ya kidijitali na ubunifu katika sekta ya fedha.

Kampeni hii itaendelea katika kipindi chote cha msimu wa sikukuu, na TCB imewahimiza wateja wake kuhuisha na kutumia kadi zao za Popote Visa ili kunufaika na ofa hiyo,Benki imesisitiza kuwa kadi hiyo inakubalika duniani kote na inatoa taarifa za miamala papo hapo, hivyo kuifanya kuwa njia salama, rahisi, na ya kisasa ya kufanya malipo ndani na nje ya nchi.



