Home KITAIFA Kamishna Jenerali Lyimo:ambao bado wanaendelea na biashara ya dawa za kulevya ...

Kamishna Jenerali Lyimo:ambao bado wanaendelea na biashara ya dawa za kulevya sheria itachukua mkondo wake

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

KAMISHINA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA), Aretas Lyimo amesema wale ambao bado wanaendelea kufanya biashara ya dawa za kulevya sheria,itawafikia na itachukua mkondo wake kwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Akizungumza leo Julai 5,2025 jijini Dar es Salaam Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo, Lyimo kwenye Maonesho ya Biashara ya 49 ya Kimataifa Sabasaba amesema lengo ni kuwapa wananchi elimu ili wajue aina ya dawa za kulevya lakini wajue unapokamatwa na dawa za kulevya sheria inasemaje kuhusu dawa hizo.

Amesema kwa mujibu wa sheria kuna vifungu vya sheria hususani kifungu namba 24 kinachoeleza kwamba yeyote yule anayehamasisha matumizi dawa za kulevya anachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.

“Wale wote watakaoendelea kutangaza, kusifia au kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya iwe kwa mavazi, nyimbo kwa jambo lolote lile linaloonesha wanasifia au wanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya hatua ya kisheria itaendelea kuchukuliwa kwa wahusika,” amesema.

Akuzungumza kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kwa sasa hali inaendelea kuwa nzuri na inaendelea kuimarika kutokana na operesheni mbalimbali zinazoendelea kufanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hali ya sasa hivi dawa za kulevya ikiwemo heron na Cocaine zimeadimika kwa kiasi kikubwa hata ukienda kwenye vijiwe ,stendi za basi na maeneo mengine huwezi kukuta wale mateja ambao tulizoea kuwaona barabarani wananing’inia.

Sasa hali imekuwa tofauti na hiyo imetokana na Serikali kuamua kuwachukua waraibu ambao wamepelekwa kwenye mfumo wa tiba ,wanapata matibabu na wanaendelea kuimarika na wanarudi katika hali zao za kawaida na wote wanatibiwa bure,”amefafanua.

Kamishna Jenerali Lyimo ameongeza kuwa kwa sasa wapo katika operesheni maalum ya kuhakikisha wanatoa elimu maalum kwa wanafunzi wa elimu ya msingi sekondari na vyuo lakini wanafanya operesheni maalum ya kukamata wale wote ambao bado wanaendelea kujihusisha na biashara ya usambazaji na uzalishaji wa dawa za kulevya.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi tunamaliza kabisa tatizo la dawa za kulevya nchini lakini wananchi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dawa za kulevya. Wanaoendelea kufanya biashara hizo waweze kuacha na wanaoingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya wasiingie kwenye matumizi ya dawa hizo.Lakini wale ambao tayari wameingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya waweze kupatiwa matibabu na Serikali inatoa huduma za matibabu bure kwa wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya,”amesema.

Pia amewaomba Watanzania waachane na biashara ya matumizi ya dawa za kulevya, waachane na uzalishaaji na usambazaji wa dawa hizo lakini wazazi wahakikishe wanalinda watoto wao wasijiingize kwenye matumizi au biashara ya dawa za kulevya ili kuhakikisha tunajenga kizazi imara na uchumi endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here