Home KITAIFA Mradi wa upanuzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kinyerezi...

Mradi wa upanuzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kinyerezi I Extension umekamilika-Naibu Waziri Salome

📌 Utaimarisha upatikanaji wa umeme Mbagala na Gongo la Mboto

📌 Majaribio yameanza; Shukurani kwa Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema kuwa mradi wa upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Kinyerezi 1 Extension umekamilika rasmi, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa Transfoma yenye uwezo wa MVA 175.

Amesema hatua hii ni muhimu kwa kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Jiji la Dar es Salaam, hususan maeneo ya Mbagala na Gongo la Mboto, ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za kukatika kwa umeme kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

Salome amesema hayo Desemba 11, 2025, wakati wa ziara yake katika vituo vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II na Ubungo III akiongeza kuwa mradi tayari umeanza majaribio (testing).

“Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa. Transfoma zimefungwa, majaribio yanaendelea, na wananchi wa Gongo la Mboto na Mbagala sasa watapata umeme wa uhakika,” Salome.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Shirika linaendelea kuboresha miundombinu yake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Amebainisha kuwa katika eneo la Kinyerezi kumefungwa Transfoma kubwa ya MVA 175, huku maeneo ya Gongo la Mboto na Mbagala yakiwekewa Transfoma ya MVA 120 ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.

Amesisitiza kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka Jiji la Dar es Salaam, hivyo miundombinu ya umeme lazima iboreshwe mara kwa mara ili kuendana na uhitaji uliopo.

“Lengo la Kinyerezi 1 Extension lilikuwa kuongeza uwezo wa kusambaza umeme unaozalishwa kuwafikia wateja wetu kwa kiwango kinachostahili,” amesema Twange.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here